Na Daudi Julian, Morogoro.
CHAMA cha makocha wa mpira wa miguu Tanzania (TAFCA) mkoa wa Morogoro kimeandaa kozi ya kati kwa makocha wa mchezo huo inayotarajiwa kuanza kufanyika Februari 26, mwaka huu, mkoani hapa.
Akizungumza na mtandao huu, katibu mkuu wa chama hicho, Hemed Mumba alisema maandalizi kwa ajili ya kozi hiyo itakayochukua siku kumi yanakwenda vizuri na kwamba tayari baadhi ya makocha wameshajiandikisha.
Mumba alisema lengo la kozi hiyo ni kuwaendeleza makocha wa mpira wa miguu mkoani Morogoro na mikoa mingine ili kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua kubwa.
Katibu huyo alisema ada inatakiwa kulipwa kwa mweka hazina wa chama au katibu mkuu katka ofisi za chama hicho zilizopo ndani ya ofisi za chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) na mshiriki ahakikishe anapewa risiti.
“Maandalizi kwa ajili ya kozi hii yanakwenda vizuri na makocha wameanza kujitokeza lakini pia milango ipo wazi hata kwa makocha walio nje ya Morogoro kuja kuchukua mafunzo haya”, alisema.
Kozi hiyo ni ya kwanza kutolewa na chama hicho chini ya uongozi mpya ulioingia madarakani hivi karibuni chini ya mwenyekiti wake, John Simkoko.