Na Bosire Boniface, Garissa
Zaidi ya Wasomali 1,000 wanaoishi katika kambi mchanganyiko ya Dadaab nchini Kenya walirejea nyumbani kipindi cha mwezi mmoja uliopita kwa msaada kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), msemaji wa shirika hilo nchini Kenya Emmanuel Nyabera aliiambia Sabahi.

Mfanyakazi wa UNHCR akipunga mkono kwa familia za Somalia zinazoondoka katika kambi ya wakimbizi ya Ifo kwenda Somalia tarehe 9 Disemba, 2014. [Bosire Boniface/Sabahi]
Urejeshwaji makwao kwa hiari, sehemu ya mpango wa majaribio wa miezi sita uliozinduliwa tarehe 8 Disemba, kufuatia makubaliano ya pande tatu yaliyotiwa saini 2013 kati ya Kenya, Somalia na UNHCR.
Ifikapo mwezi Juni, kutokana na makubaliano haya, Wasomali wanaokadiriwa kufikia 10,000 watapata msaada kurejea Luuq, Baidoa na Kismayo, Nyabera alisema, akiongezea kwamba shirika hili kwa sasa linafanya utaratibu wa maombi ya wakimbizi wengine wanaotaka kurudi nyumbani.
Huduma za msaada zinazotolewa kwa wakimbizi wanaorudi zinajumuisha msaada wa kupata usafiri salama, msaada wa fedha taslimu, usafiri na vifaa vya usafi kwa ajili ya matumizi wakati wa safari ya kurejea nyumbani, chakula na mahitaji mengine ya msingi kusaidia uendelevu wa kurudi na kuwaunganisha na jamii nchini Somalia.

Mama na watoto wake wakisubiri pamoja na wakimbizi wengine kupanda basi kurejea Somalia katika kambi ya wakimbizi ya Ifo. [Bosire Boniface/Sabahi]
Ibrahim Hussein Abdi, mwenye umri wa miaka 43, aliiambia Sabahi kwamba amewasilisha jina lake kwenye ofisi za UNHCR huko Dadaab kwa urejeshwaji nyumbani nchini Somalia kwa hiari.
Abdi, aliyewasili katika maeneo ya Dadaab na familia yake mwezi Mei 2010, alisema maisha kama mkimbizi yalikuwa na changamoto na ameiona vigumu kuzoea katika hali halisi ya ukaaji wake.